Rais Mwinyi azindua minara 42 iliyofadhiliwa na UCSAF, Zanzibar

  • 01 November, 2022
Rais Mwinyi azindua minara 42 iliyofadhiliwa na UCSAF, Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amezindua minara arobaini na mbili (42) ya mawasiliano ya simu na kituo cha TEHAMA vilivyojengwa kupitia ruzuku inayotolewa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF).
 
Katika hafla hiyo ya uzinduzi Mhe, Dkt. Mwinyi ameupongeza uongozi na watendaji wa UCSAF kwa kuhakikisha ujenzi wa miradi hiyo ya kimkakati inakamilika kwa wakati huku akiongeza kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutasaidia kutatua changamoto ya mawasiliano pamoja na kukuza uelewa wa TEHAMA kwa wananchi visiwani Zanzibar.
 
Kwa upande mwingine, Rais Mwinyi ametoa wito kwa wananchi kuwa walinzi wa miundombinu hiyo na kuwataka kuhakikisha kuwa kituo cha TEHAMA kinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
 
Naye Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye (Mb) amesema; “Lengo la miradi hii ya kimkakati ni kuhakikisha huduma za mawasiliano zinaboreshwa na kuwafikia watanzania wote kila mahali bila kujali eneo la kijiografria ambapo mtanzania yupo”.
 
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Dkt. Khalid Salum amesema kuwa uboreshaji huo wa huduma za mawasiliano unaendana na dhamira ya nchi ya kukuza uchumi wa buluu ili wavuvi na watumiaji wa bahari waweze kupata mawasiliano popote walipo katika shughuli zao za uvuvi.
 
Akitoa taarifa fupi ya utekelezaji wa miradi hiyo Mtendaji Mkuu UCSAF Bi. Justina Mashiba amesema, katika ujenzi wa minara hiyo Mfuko umetoa ruzuku ya takribani shilingi Bilioni 7  ikiwa ni sawa na ruzuku ya fedha za kitanzania milioni 164 kwa kila mnara.

Jumla ya shehia( kata) 38 zenye maeneo 42 zimefikiwa na huduma hiyo ambapo wananchi zaidi ya laki tatu wanapata huduma ya mawasiliano ya simu bila changamoto yoyote