UCSAF yaendelea kuboresha huduma ya mawasiliano vijijini

  • 25 February, 2022
UCSAF yaendelea kuboresha huduma ya mawasiliano vijijini

Naibu Waziri, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Andrea Mathew (Mb) amefanya uzinduzi wa mnara wa mawasiliano ya simu uliojengwa kwa ruzuku ya Serikali inayotolewa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF).

Mnara huo umeziduliwa katika Kata ya Loya, Kijiji cha Magulyati Wilayani Uyui Mkoani Tabora. Katika uzinduzi huo Naibu Waziri Kundo ameipongeza UCSAF kwa kuendelea kushirikiana na watoa huduma za mawasiliano ya simu ili kufikisha mawasiliano katika maeneo ya pembezoni na yale yasiyo na mvuto wa kibiashara kwa watoa huduma za mawasiliano.

Ameongeza kuwa, ufikishaji wa huduma ya mawasiliano katika katika maeneo mbalimbali ya nchi umekuwa ni chachu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii huku akisema kuwa, kuzinduliwa kwa mnara huo kutachangia kuongeza makusanyo ya mapato katika halmashauri ya wilaya ya Uyui na Mkoa wa Tabora kwa ujumla.

Akizungumza katika uzinduzi huo Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Mhe. Kisare Makori ambaye pia alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tabora amesema, kuimarika kwa mawasiliano katika wilaya ya Uyui kutachangia pia kuimarisha hali ya ulinzi na usalama kwa kuwa kumekuwepo na matukio ya uhalifu ambayo yamekuwa yakifanywa na watu katika maeneo ambayo hayana mawasiliano. 

Nae Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba amesema, hadi sasa Mfuko umesaini mikataba 1,112 ya kufikisha huduma za mawasiliano, ambapo miradi 796 imekamilika na miradi mingine 316 itakuwa imekalimilika ifikapo mwezi Julai mwaka huu. Katika Wilaya ya Uyui pekee, Mfuko unatekeleza miradi 24 ya mawasiliano ambapo hadi sasa miradi 18 yatari imekwishakamilika.

Katika kuendelea kuboresha mawasiliano katika Mkoa huo, maeneo mengine 19 yamekwisha kuainishwa na Mfuko na mchakato wa kuyafikishia mawasiliano unaendelea. Aidha Mashiba ameongeza kuwa Mfuko unatekeleza mradi wa kuiongezea uwezo minara iliyokuwa na teknolojia ya 2G pekee ambayo ni mawasiliano ya simu bila mtandao wa intaneti, sasa inaongezewa uwezo kwa kushirikiana na watoa huduma za mawasiliano ili iweze kutoa pia huduma ya intaneti