UCSAF yaendelea kuboresha mawasiliano mipakani

  • 10 January, 2023
UCSAF yaendelea kuboresha mawasiliano mipakani

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe, Nape Nnauye (Mb) amesema Serikali kupitia Wizara hiyo imedhamiria kuhakikisha kuwa, wananchi waishio mikoa yote ya mipakani wanapata huduma ya mawasiliano ya uhakika.

Mhe, Nape ameyasema hayo wakati akizindua mnara wa mawasiliano ya simu uliojengwa na kampuni ya simu ya MIC ( Tigo) kupitia ruzuku inayotolewa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ( UCSAF).

Aidha Mhe, Nnauye ameishukuru kampuni ya simu ya MIC kwa kushirikiana na UCSAF kujenga mnara huo katika kijiji cha Katuka, kata ya Msanzi wilaya wa Kalambo mkoani Rukwa. Aidha, ametoa wito kwa kampuni nyingine za simu kutumia mnara huo kutoa huduma ili kuwawezesha wananchi kupata huduma bora zaidi.

Katika uzinduzi huo Mkuu wa mkoa wa Rukwa Bi.Queen Sendiga amesema, atahakikisha kuwa miundombinu ya umeme na barabara inakamilika ili kuwezesha mnara huo kutoa huduma kama ilivyokusudiwa.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Bi.Justina Mashiba amesema, kwa kutambua changamoto ya mawasiliano katika maeneo mbalimbali nchini, UCSAF imetangaza zabuni ya kupeleka huduma za mawasiliano ambayo inatarajiwa kufunguliwa mwishoni mwa mwezi Januari  mwaka huu. Katika zabuni hiyo, minara 17 imepangwa kujengwa katika Mkoa wa Rukwa.