UCSAF yakabidhi vifaa vya TEHAMA kwa baadhi ya shule za umma nchini.

  • 15 September, 2021
UCSAF yakabidhi vifaa vya TEHAMA kwa baadhi ya shule za umma nchini.

Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umekabidhi vifaa vya TEHAMA kwa Shule ya Sekondari za umma za Tanzania Bara. Shule ya Dutwa Nkololo zilizopo katika Wilaya ya Bariadi zimepokea kompyuta 10 na printa 2 ambapo kila shule imepatiwa kompyuta 5 na pinta 1. Vifaa hivyo vimekabidhiwa kwa Mbunge wa Bariadi ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew ambaye ndiye aliyevikabidhi katika shule hizo akiambatana na Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Lupakisyo Kapange.

“TEHAMA inaenda kuchangia kukuza uchumi wa dunia na sisi Tanzania tumeona kwamba tusibaki nyuma katika kukuza matumizi ya TEHAMA kwa kuhakikisha vijana wetu wanajifunza TEHAMA kuanzia shuleni na nikiwa kama Mbunge wa Bariadi nina kila sababu ya kuwasisitiza vijana wetu kusoma kwa bidii”, amezungumza Mhandisi Kundo

Naibu Waziri huyo ametoa rai kwa wanafunzi hao kusoma kwa bidii ili kupata ufaulu mzuri katika mitihani yao ya Kitaifa na kusisitiza kuwa wanafunzi watakaopata ufualu wa daraja la kwanza la pointi 7,8,9 atawalipia ada kama alivyoahidi wakati wa kampeni ya uchaguzi mwaka 2020.

Nae Mbunge wa viti maalum wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Santiel Kirumba amekabidhi vifaa hivyo vya TEHAMA zikiwemo Kompyuta 5, Printa 1 pamoja na spika zake vyenye thamani ya milioni 15 kwa ajili ya shule ya Sekondari ya Wasichana Kishapu 'Kishapu Girls' mkoani Shinyanga.

Pia alizungumzia mradi wa wasichana na TEHAMA unaotekelezwa na UCSAF ambao unalenga kuwawezesha na kuwajengea uwezo watoto wa kike katika TEHAMA ndio maana katika upelekaji wa vifaa vya TEHAMA katika shule za sekondari Mfuko huo unaangazia na Shule za Sekondari za wasichana.

“Wizara kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote tuna kipengele kingine cha kuwawezesha watoto wa kike na TEHAMA ili kuwajengea uwezo na hatimaye kutengeneza wataalam wa TEHAMA wengi zaidi nchini kwa sababu mpaka sasa wataalam wa TEHAMA wanawake ni wachache kuliko wa kiume lengo letu ni kwamba tunapoongelea 50 kwa 50 ionekane kwa vitendo", alisema Mhandisi Kundo.

Kwa Upande wa Mkuu wa Uendeshaji wa UCSAF Eng. Albert Richard amesema moja ya majukumu yanayotekelezwa na Mfuko huo ni kupeleka vifaa vya TEHAMA katika shule za umma ili kuendelea kuinua matumizi ya TEHAMA nchini. Naye Mwalimu Mekrina Bonifasi wa Shule ya Sekondari Dutwa amesema kuwa msaada huo wa kompyuta utakuwa chachu ya ufaulu na utasaidia sana katika ufundishaji na ujifunzaji kwa wanafunzi hasa ukizangatia kuwa kwa sasa shule hiyo ina wanafunzi wa kidato cha kwanza wapatao 280 ambao wanasoma somo la kompyuta na watafanya mtihani wa Taifa 2022 kwa mara ya kwanza.