Ufunguzi wa mafunzo ya TEHAMA, Naibu Waziri TAMISEMI aipongeza UCSAF.

  • 25 October, 2021
Ufunguzi wa mafunzo ya TEHAMA, Naibu Waziri TAMISEMI aipongeza UCSAF.

Naibu Waziri wa TAMISEMI, David Silinde ameupongeza Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutekeleza Sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 kwa kutoa mafunzo ya TEHAMA kwa walimu wa shule za msingi na sekondari nchini.

Naibu Waziri, Silinde ameyasema hayo katika ufunguzi wa mafunzo ya TEHAMA kwa walimu yaliyoandaliwa na UCSAF kwa kushirikiana na taasisi ya Teknolojia ya Dar es salaam (DIT) jijini Dar es salaam. Ameongeza kwa kusema kuwa Serikali inatambua umuhimu wa mafunzo kama hayo na kuahidi kuimarisha muundo na utaratibu wa ufundishaji wa masomo ya sayansi na Teknolojia katika ngazi zote za elimu na mafunzo kwa kuhakikisha kuwa inatumia teknolojia katika utoaji wa elimu.

"Kupitia sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014, Serikali itahakikisha vifaa, nyenzo na zana stahiki za kufundishia na kujifunzia zinatosheleza kulingana na mahitaji na maendeleo ya sayansi na teknolojia katika ngazi zote" amesema Naibu Waziri huyo.

Kwa upande wake mkuu wa Taasisi ya DIT, Profesa Preksedis Ndomba ameishukuru UCSAF kwa kuandaa mafunzo hayo na kuongeza kuwa lengo ni kuwajengea walimu hao uwezo wa kutatua matatizo madogo madogo ya kitehama katika vifaa vilivyotolewa katika shule zao na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote kwa lengo la kuwapatia wanafunzi nafasi ya kujifunza kutumia vifaa hivyo katika hatua za awali ili kuwajengea uwezo,maarifa, ujuzi na ushindani.

Mafunzo haya yanafanyika kwa wiki moja katika vituo vitatu tofauti, taasisi ya Teknolojia Dar es salaam (DIT), Chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) ambapo jumla ya walimu 650 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar watapatiwa mafunzo hayo.