WAZIRI Mawasiliano Zanzibar afanya ziara ya kikazi UCSAF.

  • 25 October, 2021
WAZIRI Mawasiliano Zanzibar afanya ziara ya kikazi UCSAF.

WAZIRI wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Rahma Kassim Ali amefanya ziara ya kikazi katika ofisi za Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa lengo la kupata taarifa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekezwa na Mfuko huo. Akifanya wasilisho mbele ya Waziri Rahma, Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba amesema, kwa upande wa Zanzibar, Mfuko umekamilisha ujenzi wa kituo cha miito ya dharura (emergency call centre) kituo ambacho kitatumika kuratibu matukio ya dharura.

Aidha ameogeza kuwa, shule 13 za umma za Visiwani humo zimenufaika na awamu ya tano ya utekelezaji wa mradi wa kuunganisha shule na mtandao wa intaneti na kuzipatia shule hizo vifaa vya TEHAMA, ambapo kila shule ilipatiwa kompyuta tano. Mtendaji Mkuu, ameongezea kuwa walimu wa shule za umma kutoka Zanzibar pia wananufaika na mafunzo ya TEHAMA kwa walimu ambayo yanatolewa na UCSAF kwa kushirikiana na vyuo vikuu mbalimbali nchini.

Akizungumza baada ya wasilisho hilo, Waziri Rahma ameipongeza UCSAF huku akitoa wito wa kuhakikisha kuwa Mfuko unafikia maeneo yenye changamoto za mawasiliano hasa katika kisiwa cha Pemba ambako wananchi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto hiyo. Pia ametoa wito wa kutoa kipaumbele kwa watu wenye mahitaji maalumu katika kuwapatia mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili nao waweze kunufaika na huduma hiyo.

"Kisiwa kile kwa upande wa mawasiliano bado hakijawa vizuri kwa hiyo ninyi UCSAF kwa vile ni mfuko wa mawasiliano fanyeni jambo, pia tunapoenda mbele katika mawasiliano hatupaswi kuwaacha wenzetu hawa watu wenye ulemavu kwani wakipatiwa mafunzo watakuwa na uelewa zaidi,"amesema Waziri Rahma.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Justina Mashiba, amepokea maelekezo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi ili kuhakikisha huduma ya mawasiliano inawafikia wananchi wote wa Zanzibar.

"Mfuko unaendelea kupambana ili kuweza kuhakikisha huduma ya mawasiliano inapatikana kote,na lengo ni kila sehemu kuwe na mawasiliano,"amesema Mashiba.

Katika ziara hiyo, Waziri Rahma pia amekagua mradi wa ujenzi wa ofisi za Mfuko huo zinazojengwa katika eneo la Njedengwa jijini hapa.