Waziri Mkuu aipongeza UCSAF kwa kuboresha huduma za mawasiliano na kukuza uelewa wa TEHAMA.
- 25 October, 2021
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa ameupongeza Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ( UCSAF) kwa kuendelea kuboresha huduma za mawasiliano na kukuza uelewa wa matumizi ya TEHAMA na vifaa vya TEHAMA nchini.
Waziri Mkuu Majaliwa, ameyasema hayo alipotembelea banda la maonyesho la UCSAF katika maonyesho yaliyofanyika jijini Arusha ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya mkutano wa tano wa mwaka wa TEHAMA nchini, na kupata taarifa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali kutoka kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko huo, Justina Mashiba.
Aidha, ametoa wito kwa UCSAF kuendelea kuwafikia wananchi ambao wameachwa nyuma kiteknolojia ili kuendelea kukuza sekta ya TEHAMA kwa kuwa Tanzania imedhamiria kufanikisha mageuzi makubwa katika uchumi wa kiditali kwa kuhakikisha kuwa mifumo ya TEHAMA inazifikia jamii zote za mijini na vijijini. Lengo likiwa ni hadi kufikia mwaka 2025 wataalam wa TEHAMA nchini wafikie elfu tano (5,000) ili Tanzania iweze kumudu ushindani unaondelea duniani.
Miongoni mwa Viongozi walioambatana na Waziri Mkuu walikuwa ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe, Dkt. Ashatu Kijaji, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt.Zainab Chaula, Naibu Katibu Mkuu Dkt. Jim Yonazi na Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa. Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella, Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya miundombinu Seleman Kakoso na Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Mhe Mrisho Gambo.
Mhe. Majaliwa alikuwa mgeni rasmi katika Mkutano wa tano wa Mwaka wa TEHAMA uliofanyika katika kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha( AICC).