Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF)

TANGAZO LA KUWASILISHA MAOMBI YA RUZUKU KWA AJILI YA UJENZI NA UBORESHAJI WA VITUO VYA REDIO NA TELEVISHENI JAMII KWA MWAKA WA FEDHA 2027/28

23 October, 2026
  1. UTANGULIZI

Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ulianzishwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Sheria ya Mawasiliano kwa Wote (UCSA Act), Sura ya 422 na ulianza kazi rasmi tarehe 1 Julai 2009. Mfuko una jukumu la kuwezesha upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi wanaoishi katika maeneo ya vijijini na mijini yasiyo na huduma hizo au yenye huduma hafifu.

Katika kutekeleza majukumu hayo, UCSAF hutoa ruzuku kwa ajili ya ujenzi na kuboresha miundombinu na upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya simu, utangazaji, posta na TEHAMA (teknolojia ya habari na mawasiliano). Kupitia ruzuku kwa Redio na Televisheni Jamii, Mfuko unalenga kuongeza upatikanaji wa taarifa na huduma za utangazaji zinazokidhi mahitaji ya jamii, hususan katika maeneo yasiyo na huduma hizo au yenye huduma hafifu.

UCSAF inatarajia kutenga fedha katika Mpango na Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2027/28 ili kutoa ruzuku kwa ajili ya kuwezesha ujenzi, upanuzi au uboreshaji wa miundombinu ya vituo vya Redio na Televisheni Jamii katika maeneo yenye uhitaji.

Hivyo, UCSAF inazikaribisha halmashauri, mashirika yasiyo ya kiserikali, taasisi na asasi za kijamii, taasisi za elimu na taasisi nyingine zisizo za kibiashara zinazokidhi vigezo kuwasilisha maombi ya ruzuku kwa ajili ya miradi hiyo. Maombi hayo yatatumika kubaini miradi inayostahili kuzingatiwa katika Mpango na Bajeti ya UCSAF kwa Mwaka wa Fedha 2027/28.

Ruzuku itatolewa kwa vituo vitano (5) vitakavyokidhi vigezo vilivyowekwa kwenye tangazo hili kwa kuzingatia matokeo ya tathmini ya maombi yatakayowasilishwa na bajeti itakayoidhinishwa.

Mwisho wa kuwasilisha maombi ni tarehe 30 Novemba 2026 saa 14:30 kwa saa za Afrika Mashariki.

  1. LENGO LA UTOAJI RUZUKU
    1. Lengo kuu

Kuongeza upatikanaji wa huduma za Redio na Televisheni Jamii katika maeneo yenye uhitaji kwa kugharamia uwekezaji wa miundombinu na vifaa vya kuanzisha, kupanua au kuboresha vituo hivyo.

    1. Malengo mahususi
  1. Kupanua ufikivu wa huduma za Redio na Televisheni Jamii katika maeneo yasiyohudumiwa au yenye huduma zisizotosheleza, kupitia uwekezaji katika miundombinu na vifaa vya utangazaji;
  2. Kuwezesha uanzishaji wa vituo vipya vya Redio na Televisheni Jamii kwa kusaidia gharama za miundombinu na vifaa vinavyohitajika;
  3. Kuimarisha uwezo na ubora wa kiufundi wa vituo vya Redio na Televisheni Jamii kupitia upanuzi au uboreshaji wa miundombinu na vifaa vya utangazaji kulingana na upatikanaji wa fedha na miradi inayokidhi vigezo vya UCSAF; na
  4. Kuelekeza ruzuku katika uwekezaji wenye manufaa kwa jamii, unaozingatia uhitaji wa huduma na uwezo wa waombaji kugharamia uendeshaji na matengenezo baada ya uwekezaji.
  1. MIRADI NA GHARAMA ZINAZOWEZA KUFADHILIWA

Maombi yanaweza kuhusisha moja au zaidi ya maeneo yafuatayo:

  1. Ujenzi au uboreshaji wa studio za Redio na Televisheni Jamii;
  2. Ujenzi au uboreshaji wa miundombinu (minara) ya kurushia matangazo inayohusiana moja kwa moja na huduma ya Redio na Televisheni Jamii;
  3. Ununuzi na usimikaji wa mitambo ya utangazaji, antena, laini ya mawasiliano (transmission line) na vifaa saidizi;
  4. Vifaa vya msingi vya uzalishaji, urushaji na ufuatiliaji wa matangazo;
  5. Mifumo ya umeme ya uhakika, ikiwemo UPS, jenereta au nishati mbadala pale inapohitajika;
  6. Huduma za usanifu (Technical Site Survey), upimaji wa kiufundi, usimikaji, majaribio na uanzishaji wa huduma; na
  7. Vipengele vingine vya mtaji (CAPEX) vinavyohusiana moja kwa moja na uanzishaji au uboreshaji wa huduma za Redio na Televisheni Jamii.

Ruzuku haitagharamia matumizi ya kawaida ya uendeshaji, ikiwemo mishahara, posho, kodi ya pango, gharama za kawaida za uzalishaji wa maudhui, matangazo ya kibiashara, madeni ya nyuma au matumizi yasiyohusiana moja kwa moja na gharama za mtaji wa mradi ulioidhinishwa.

  1. MAENEO YENYE KIPAUMBELE
  1. Maeneo yasiyo na huduma ya Redio na Televisheni Jamii;
  2. Maeneo yenye huduma duni, isiyoaminika au isiyofikia sehemu kubwa ya wananchi;
  3. Maeneo ya vijijini, pembezoni, mipakani, visiwani au yenye changamoto za kijiografia;
  4. Maeneo yenye uhitaji mkubwa wa taarifa za maendeleo, elimu, afya, kilimo, uvuvi, ufugaji, mazingira, tahadhari za majanga, utawala bora na huduma nyingine za kijamii;
  5. Maeneo ambayo hayana mvuto wa kutosha wa kibiashara kwa watoa huduma;
  6. Maeneo yenye jamii zinazokabiliwa na changamoto maalum za upatikanaji wa taarifa na huduma za utangazaji; na
  7. Maeneo mengine yenye umuhimu na maslahi kwa Taifa.
  1. WAOMBAJI WANAOSTAHILI

Ifuatayo ni orodha ya Makundi ya waombaji wanaostahili kuomba ruzuku hii:

  1. Halmashauri za Wilaya;
  2. Halmashauri za Miji;
  3. Manispaa na Majiji;
  4. Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs);
  5. Taasisi na asasi za kijamii;
  6. Taasisi za elimu; na
  7. Taasisi nyingine zisizo za kibiashara zenye sifa na mamlaka ya kisheria ya kutekeleza shughuli husika.
    1. Sifa za lazima

Ili mwombaji astahili kuomba na kuzingatiwa kupata ruzuku, atalazimika kutimiza sifa zote za msingi zilizoainishwa hapa chini. Kutotimiza mojawapo ya sifa hizi kunaweza kusababisha maombi husika kutoendelea na hatua zinazofuata za tathmini. Mwombaji anatakiwa:

  1. Kuwa na usajili halali au mamlaka ya kisheria ya kuendesha shughuli zake.
  2. Kuwa na leseni halali ya utangazaji au ushahidi rasmi wa hatua ya kupata leseni/kibali kutoka TCRA;
  3. Kuwa na eneo la mradi lililobainishwa wazi pamoja na ushahidi wa uhitaji wa huduma inayoombewa;
  4. Kuwa na mpango wa uendelevu wa kituo baada ya ruzuku;
  5. Kuwasilisha azimio la mamlaka inayosimamia taasisi hiyo au uthibitisho wa ushirikishwaji wa jamii inayohusika;
  6. Kukubali kufanyiwa tathmini ya awali, ukaguzi wa kiufundi, ufuatiliaji na tathmini wakati na baada ya utekelezaji; na
  7. Kuwa tayari kusaini mkataba na kutekeleza masharti ya UCSAF.
    1. Sababu za kutostahili

Maombi yanaweza kuondolewa katika tathmini au kukataliwa iwapo mwombaji:

  1. Amewasilisha taarifa na nyaraka zisizo sahihi au zilizoghushiwa;
  2. Amependekeza mradi unaotanguliza maslahi binafsi au ya biashara kuliko maslahi ya jamii;
  3. Ana mgogoro wa kisheria au kiutawala katika taasisi husika unaoweza kuathiri utekelezaji wa mradi;
  4. Alishindwa kutekeleza ipasavyo mradi wa awali wa UCSAF bila sababu za msingi;
  5. Hajakidhi masharti ya leseni, usajili au vibali vinavyohitajika; na
  6. Ana mgongano wa maslahi na UCSAF.
  1. Nyaraka za Kuwasilisha

Mwombaji awasilishe nyaraka zifuatazo kwa kadiri zitakavyomhusu:

  1. Barua rasmi ya maombi ya ruzuku;
  2. Andiko dhana au pendekezo la mradi kwa kutumia muundo uliopo katika kwenye Sehemu ya 7 (Section 7);
  3. Cheti cha usajili au uthibitisho wa mamlaka ya kisheria;
  4. Leseni ya TCRA au ushahidi wa hatua ya kupata leseni/kibali, pale inapokubalika;
  5. Azimio la Halmashauri, Bodi, Kamati ya jamii au chombo husika kinachoidhinisha mradi;
  6. Ushahidi wa ushirikishwaji wa jamii na mahitaji ya huduma;
  7. Taarifa ya eneo la mradi, ikiwemo Mkoa, Wilaya, Kata, Kijiji/Mtaa na makadirio ya wananchi watakaonufaika;
  8. Mpango wa uendelevu wa kituo;
  9. Makadirio ya gharama na maelezo ya mchango wa mwombaji, kama upo; na
  10. Nyaraka nyingine zitakazoainishwa na UCSAF katika tangazo la mwaka husika.

Maombi yasiyo na nyaraka muhimu yanaweza kuondolewa katika hatua ya awali ya tathmini. UCSAF inaweza kuomba ufafanuzi au nyaraka za ziada bila kubadilisha msingi wa maombi yaliyowasilishwa.

  1. MUUNDO WA ANDIKO DHANA AU PENDEKEZO LA MRADI

Andiko dhana liainishe yafuatayo:

  1. Jina la mwombaji, aina ya usajili, namba ya usajili na anwani za mawasiliano;
  2. Eneo la mradi: Mkoa, Wilaya, Kata, Kijiji/Mtaa na maelezo mafupi ya eneo;
  3. Maelezo ya tatizo/changamoto: kiwango cha ukosefu au uduni wa huduma na ushahidi wa uhitaji;
  4. Uhalali wa mradi: kwa nini mradi unahitajika na jinsi unavyoendana na malengo ya UCSAF;
  5. Malengo ya mradi: lengo kuu na malengo mahsusi;
  6. Walengwa na makadirio ya idadi ya watu watakaofikiwa;
  7. Maelezo ya kiufundi ya awali: eneo la studio, mnara, vifaa vinavyohitajika na mfumo wa umeme;
  8. Manufaa yanayotarajiwa kwa jamii;
  9. Mpango wa uendelevu wa huduma;
  10. Mpango wa utekelezaji na ratiba ya awali;
  11. Makadirio ya gharama na mchango wa mwombaji/wadau, kama upo; na
  12. Viambatisho vya uthibitisho.
  1. TATHMINI YA MAOMBI NA UTOAJI WA RUZUKU

Tathmini itahusisha uhakiki wa ukamilifu wa maombi na sifa za lazima, uchambuzi wa kiufundi, kifedha na kijamii, pamoja na uendelevu wa mradi. Ziara ya eneo itafanyika inapohitajika. Miradi itapangwa kwa kuzingatia alama za tathmini, kipaumbele cha eneo na bajeti iliyopo.

Vigezo vya kina, mgawanyo wa alama na masharti ya ruzuku vimeainishwa kwenye Jedwali hapa chini.

Na.

Kigezo

Alama za juu

  1.  

Uhitaji wa huduma katika eneo

30

  1.  

Madhumuni ya mradi na manufaa kwa jamii

20

  1.  

Utayari wa kisheria na kitaasisi

10

  1.  

Uwezekano wa kiufundi

10

  1.  

Uendelevu wa huduma

10

  1.  

Thamani ya fedha itakayotolewa

10

  1.  

Ujumuishi na ushiriki wa jamii

5

  1.  

Uzingatiaji wa mazingira na usalama

5

 

Jumla

100

Uamuzi wa utoaji wa ruzuku utategemea bajeti iliyoidhinishwa, matokeo ya tathmini na kutimizwa kwa masharti husika.

  1. UKOMO WA KUWASILISHA MAOMBI

Maombi ya ruzuku yawasilishwe kabla au ifikapo tarehe 30 Novemba 2026 saa 8:30 Mchana kwa saa za Afrika Mashariki. Maombi yatakayowasilishwa baada ya muda huo hayatapokelewa kwa ajili ya tathmini. Hivyo, waombaji wanashauriwa kuwasilisha maombi mapema.

Aidha, maombi yatakayopokelewa yatafanyiwa kazi kwa kufuata mtiririko ulioainishwa kwenye Jedwali hapo chini.

MUDA

SHUGHULI

MHUSIKA

23 Oktoba 2026

Kutolewa kwa tangazo la kuitisha maombi ya ruzuku kwa ajili ya ujenzi na uboreshaji wa vituo vya Redio na Televisheni Jamii.

Sekretarieti ya Mfuko

24 Oktoba - 29 Novemba 2026

Kuandaa na kuwasilisha maombi ya ruzuku pamoja na nyaraka zinazohitajika kwa mujibu wa tangazo na Mwongozo wa Utoaji wa Ruzuku.

Waombaji wa ruzuku

30 Novemba 2026

Mwisho ya kupokea maombi ya ruzuku.

Sekretarieti ya Mfuko

1 - 5 Disemba 2026

Uchambuzi wa awali wa maombi, ukijumuisha uhakiki wa ukamilifu wa maombi na nyaraka pamoja na uchambuzi wa sifa za lazima za mwombaji na mradi.

Sekretarieti ya Mfuko

6 - 19 Disemba 2026

Uchambuzi wa kina wa maombi, ukijumuisha tathmini ya kiufundi, kifedha, kijamii na uendelevu wa mradi; ziara ya eneo (Technical Site Survey) inapohitajika; utoaji wa alama kwa kutumia vigezo vilivyoainishwa katika Mwongozo; na upangaji wa waombaji kwa kuzingatia alama, kipaumbele cha eneo na bajeti iliyopo.

Kamati ya Tathmnini

20 Disemba 2026

Kuwasilisha taarifa ya uchambuzi na mapendekezo ya kitaalamu kuhusu maombi ya ruzuku kwa ajili ya uamuzi.

Kamati ya Tathmini

23 Disemba 2026

Kuhakiki taarifa ya uchambuzi wa maombi ya ruzuku na orodha ya miradi iliyopendekezwa kupatiwa ruzuku kabla ya kuwasilishwa kwa Mtendaji Mkuu.

Menejimenti ya Mfuko

28 Disemba 2026

Kufanya uamuzi kuhusu maombi ya ruzuku yatakayoidhinishwa na yale yatakayokataliwa kwa kuzingatia vigezo, masharti ya utoaji wa ruzuku na bajeti iliyopo.

Mtendaji Mkuu

31 Disemba 2026

Kuwajulisha waombaji matokeo ya maombi yao ya ruzuku.

Sekretarieti ya Mfuko

14 Januari 2027

Kupokea na kushughulikia malalamiko ya maandishi kuhusu ukiukwaji wa taratibu za utoaji wa ruzuku.

Sekretarieti ya Mfuko

21 Januari 2027

Kusaini Hati ya Makubaliano (MoU) ya utoaji ruzuku na wanufaika walioidhinishwa.

Sekretarieti ya Mfuko na wanufaika wa ruzuku

1 Julai 2027

Kuanza utekelezaji wa miradi iliyoidhinishwa na kupatiwa ruzuku kwa mwaka wa fedha 2027/28.

Wanufaika wa ruzuku

 

  1. NAMNA YA KUWASILISHA MAOMBI

Mwombaji awasilishe barua ya maombi, andiko la mradi na nyaraka zote zinazomhusu kama zilizoainishwa katika Sehemu ya 6.

Maombi yawasilishwe kwa njia ya barua pepe, kwa mkono (in person), au kupitia anuani ya posta.

Mwombaji anatakiwa kuandaa na kuwasilisha kwa pamoja:

  1. Barua ya maombi;
  2. Andiko dhana/pendekezo la mradi;
  3. Cheti cha usajili au uthibitisho wa mamlaka ya kisheria;
  4. Leseni/kibali cha TCRA au ushahidi wa hatua ya kupata leseni;
  5. Azimio la mamlaka husika au jamii;
  6. Ushahidi wa ushirikishwaji wa jamii;
  7. Mpango wa uendelevu wa huduma;
  8. Makadirio ya gharama;
  9. Taarifa za eneo la mradi; na
  10. Nyaraka nyingine kwa mujibu wa tangazo.

 

Maombi yaelekezwe kwa:

Afisa Mtendaji Mkuu,

Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF),

Jengo la UCSAF,

S.L.P 1957,

10 Barabara ya UCSAF,

41107 DODOMA.

Baruapepe: ceo@ucsaf.go.tz

 

Kichwa cha barua au barua pepe kiwe “Maombi ya ruzuku kwa ajili ya Redio na Televisheni Jamii kwa mwaka wa fedha 2027/28.”

  1. MALALAMIKO KUHUSU MCHAKATO

Mwombaji asiyeridhika na mchakato wa utoaji ruzuku anaweza kuwasilisha malalamiko kwa maandishi kwa Mtendaji Mkuu UCSAF kupitia barua pepe ceo@ucsaf.go.tz au anwani iliyoainishwa hapo juu kabla au ifikapo tarehe 21 Disemba 2026. Malalamiko yahusu kasoro za kiutaratibu, makosa ya wazi ya tathmini au ukiukwaji wa masharti ya Mwongozo huu. Mlalamikaji abainishe maombi husika, hoja za malalamiko na ushahidi unaounga mkono hoja hizo. Malalamiko hayatatumika kuwasilisha pendekezo jipya au kubadilisha taarifa za maombi baada ya muda wa kuwasilisha maombi kuisha.

  1. MAWASILIANO KWA UFAFANUZI

Kwa ufafanuzi kuhusu tangazo hili, wasiliana na UCSAF kwa simu +255 26 2965771 au baruapepe ceo@ucsaf.go.tz.

 

IMETOLEWA NA:
AFISA MTENDAJI MKUU
MFUKO WA MAWASILIANO KWA WOTE

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Je, una swali lolote kuhusu Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF)? Faili Maoni na Malalamiko! Universal Communications Service Access Fund Ripoti Hapa
Tuma malalamiko na mrejesho wako